2 Tim 4:6-8
Sikia mstari wa sita. Assemavyo kwa ujasiri mkubwa akisema alivyokuwa tayari kumiminwa kama dhabihu, yaani kukutana na mauti.
Kiimani Paulo alitamka hivyo maana alikuwa ameweka mambo yake yote yahusuyo uhusiano wake na Mungu sawa. Hatua hiyo ndiyo iliyomsukuma kuwa tayari kukutana na mauti bila woga.
Mimi na wewe ili tukutane na mauti bila woga, ni muhimu tuhakikishe Yesu ni Mwokozi na Bwana wetu kama njia pekee ya kuwa na uhusiano sahihi na Mungu.
II.
Pili Paulo aliitazama huduma yake akaona alivyokuwa ameikamilisha vizuri (mst.7). Naamini Paulo alikumbuka maneno aliyowaandikia Warumi katika 13:36 yasemayo, “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.”
Paulo aliamini mtu akiisha kamilisha huduma aliyopewa na Mungu, kifuatacho si kingine bali kulala mauti.
Wapendwa wetu wanaotutangulia wanatwaliwa na Bwana maana wametimiza kazi waliyokuwa wamepewa kufanya. Kama kawaida mtu baada ya kumaliza kazi huwa ni kupumzika. Kwa hiyo kwetu wakristo, mauti ni mapumziko tukisubiri siku ya kupewa taji.
Amepumzika baada ya kuwa ametumikia shauri la Bwana vizuri katika kipindi cha uhai wake katika mwili huu. Ukweli huu usipingika hutupatia faraja kubwa sisi wafiwa.
III.
Jambo la tatu aliloliona Paulo mbele yake ni taji ya haki atakayoipokea kutoka kwa Kristo mwenyewe (mst. 8). Paulo anasema, “Tena si mimi peke yangu bali pamoja na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake Kristo.” Mmoja wao ni wewe.
Ndugu wafiwa, marafiki na sisi sote. Aliyefariki ameishi maisha ya utayari na uhakika wa kuingia mbinguni kwa sababu kuu ya msingi. Alimwamini Yesu Kristo kuwa Mwokozi na Mtawala wa maisha yake;
Uamuzi wake huo ndio uliompa nguvu, kwa neema yake Kristo, kuwa na ushuhuda kama unaoshuhudiwa na watu wengi. Aliyefariki amekuwa na nguvu za kuvipiga vita vya kiroho vizuri, mwendo wa ukristo ameukamilishi. Na hadi anakutana na mauti, aliyefariki alikuwa ameilinda imani kuwa Yesu pekee ndiye Njia, Kweli na Uzima.
Aliyefariki amelala lakini safari yake ya imani itaendelea kukumbukwa na wengi.
By Archbishop Daniel Bugayo Nungwana
