Tumepewa Uwezo Juu ya Kuyakabili Majaribu

Mwandishi wa kitabu cha Yakobo ametajwa wazi wazi kuwa ni Yakobo aliyekuwa nduguye Yesu (mst. 1:1). Na waandikiwa wanatajwa kuwa zile kabila 12 za Waisrael watu waliokuwa wametawanyika miongoni mwa mataifa mengine kutokana na majaribu mbali mbali (mst. 1:2).

Hii ndiyo maana Yakobo anawaita waandikiwa hawa “ndugu zangu” kutokana na uhusiano wake na Yesu. Mistari minne ya kwanza ya kitabu hiki inazungumzia juu ya majaribu mbali mbali yampatayo Mkristo (Waisraeli) [1:2b]. Na katika mistari hii inayofuata (mst. 5-11) inasema hasa juu ya uwezo tulio nao katika kuyakabili majaribu. Tunasoma katika 1:5-11 kwamba TUMEPEWA UWEZO WA KUYAKABILI MAJARIBU.

1. Tunaweza tukayakabili majaribu kwanza iwapo tutaomba hekima kutoka kwa Mungu (mst 5-8)

Yakobo anawaambia Waisraeli kuwa mtu alipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu. Mtu huyu anapungukiwa hekima akiwa katikati ya majaribu. Mtu anapozungukwa majaribu, shida na taabu ni rahisi sana kukosa hekima. (mfano) Baba aliyezidiwa njaa hata akavamia maziwa ya mkewe aliyekuwa akinyonyesha wakati huo wa njaa kali…

Yakobo anawashauri wasomaji wa barua yake waombe dua kwa Mungu ya kupata hekima. Swali, kwa nini dua hii imwendee Mungu tu? Yakobo atoa sababu akisema Mungu hana ubaguzi. Huwapatia wale wamwombao bila ubaguzi bali kwa ukarimu. Ila sharti la kupokea kile tuliombalo kwa Mungu hadi tuombe kwa Imani, tuombe pasipo shaka yoyote. Mungu wetu Yakobo anasema hafurahishwi na mtu aliye na mashaka.

Mtu kama huyo anamfananisha na wimbi la bahari linalochukuliwa na upepo na kupeperushwa huku na huku. Mtu asiyekuwa na Imani kwa lile aliombalo kwa Mungu asitegemee kupokea jema kutoka kwa Mungu. Moyo wa kusita-sita katika Biblia daima hauna sifa nzuri.

Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa akizungumza na Kanisa la saba huko Asia – Kanisa la Laodikia lilikuwa na moyo wa kusita-sita. Kusita-sita na kuwa uvuguvugu kutokuwa baridi kamili au wa moto kamili. Yesu aliliambia kanisa hilo Ufunuo 3:16, “…nitakutapika utoke katika kinywa changu.”

Uvuguvugu wa kanisa la Laodikia ulisababishwa hasa na utajiri wake. Pili wingi wa viwanda vya nguo, na tatu sifa ya kuwa na watumwa wengi. Bila kuwa na hekima itokayo kwa Mungu ni rahisi sana kuanguka dhambini wakati majaribu yanapotufikia. Hekima tunayoisema hapa si ya ujanja wa kibinadamu hata kidogo. Bali ni ule utii na heshima kwa Mungu kwani Mungu ni asili ya hekima ya kweli naye huwapa watu wake wanaoitafuta (Mithali 1:7; 2:6; 9:10).

Hekima isiyotoka kwa Mungu daima inaweza kuwa na ubinafsi pamoja na kutowajali watu, na Mungu. Hekima ya kibinadamu imejaa wivu na udanganyifu, bali hekima itokayo kwa Mungu alama yake ni unyenyekevu, unyoofu na hamu ya kuwasaidia wengine. Tusisahau kuwa hekima ya kibinadamu ina kikomo lakini hekima itokayo kwa Mungu haichuji wala haina mwisho maana aitoaye kwetu hana mwisho.

Katika hekima yake Mungu aliumba ulimwengu na kwa hekima yake anautawala ulimwengu wote (Zab 104:24, Mith 3:19, Ufun 7:12). Kutokana na hekima yake Mungu ametuokoa na mauti ya pili. Katika hekima yake, leo tunaishi kwa amani. Kwa hiyo, ili tuweze kuyakabili majaribu ambayo hatimaye yanaweza kutuangusha dhambini, tuombeni hekima kutoka kwa Mungu. Tuonyesheni matumaini yetu katika kumtegemea Mungu daima. Mtu mwenye hekima humtegemea Mungu katika kila jambo. Humwomba Mungu katika kila jambo. Humshukuru Mungu katika kila jambo. Humtukuza Mungu katika kila neno.

2. Tunaweza tu kuyakabili majaribu si wakati tunapoomba tu hekima kutoka kwa Mungu bali pili wakati tunaomba kuwa na unyenyekevu (vv 9-11)

Kuwa tajiri si dhambi, na kuwa maskini si kusema kuwa mtu huyo kalaaniwa; hata kidogo. Yakobo katika mst. 9 anaposema “Lakini ndugu asiyekuwa na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa.” Maana yake hasa ni nini?

Maana yake ni kwamba, Mkristo atesekaye kutokana na jaribu la ufukara anapaswa afurahie hali hiyo endapo inamfanya awe mnyenyekevu mbele za Bwana. Hali kadhalika, tajiri aliye Mkristo anapoingia katika majaribu ya kuishiwa na mali afurahi iwapo hali hiyo inamfanya kunyenyekea mbele za Bwana.

Fundisho kubwa hapa ni kwamba, Mkristo usipotukuzwa hapa duniani, furahi tu maana utukufu mkubwa unakusubiri mbinguni siku tutakapoketi pamoja na Kristo.

Tena Mkristo aliye tajiri apaswa kufurahi anapotambua kuwa mali aliyo nayo si ya thamani kama utajiri alio nao katika Kristo Masiyah. Kwani sisi wakristo wote tajiri kwa masikini tuna utajiri wa pekee mno kutoka kwa Mungu. Kwanza utajiri kutoka kwa Mungu Baba kutuita sisi watoto wake Waefeso 1:4-6. Utajiri wa kuchaguliwa kuwa wana wa Mungu Yohana 15:16. Utajiri tuupatao kutoka kwa Mungu Mwana (Waefeso 1:7-12).

Yeye alitukomboa (mst.7a) kutoka katika utumwa. Yeye hutusamehe dhambi zetu. Yeye hutuonyesha mapenzi yake Mungu. Yeye ametufanya kuwa warithi pamoja naye.

Utajiri tuupatao kutoka kwa Roho Mtakatifu – kule kutuweka mhuri kuwa mali yake (mst. 13-14).

Tukiyajua haya, tutapenda kuwa na maisha ya unyenyekevu wakati wote katika hali yoyote ile.

By Archbishop Daniel Bugayo Nungwana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *